U hali gani mpenzi msomaji wetu wa mtandao huu wa dira ya mafanikio, tukualike kwa mara nyingine katika kipindi hiki cha mafanikio talk ambacho hukujia kila siku ya jumanne, ambapo siku ya leo tupo na ndugu yetu SHABANI SAIDI kutokea pale Dodoma ambapo atukumbusha mambo ya muhimu ya kuzingatia katika biashara.
Ambapo alieleza ya kwamba katika biashara lengo kubwa ni kupata wateja zaidi, na katika hili wengi wamekuwa hawafahamu, wamekuwa wakizani ya kwamba lengo la kufanikiwa katika biashara ni kupata fedha pekee, lakini ukweli ni kwamba ukiwa na lengo hilo pekee utakuwa unakosea sana.
Kwani katika biashara ni lazima uweze kuwa mbunifu kila wakati, na ukiwa mbunifu kutakuwa na ongezeko la wateja na ongezeko la wateja hilo ndilo litalokufanya uweze kupata fedha, na fedha hizo zitakufanya uweze kuwa bora katika kukuza biashara yako.
Zifuatazo Ndizo Siri Sita Za Kuanzisha Biashara Yenye Mafanikio.
1. Kuwa na wazo bora la biashara.
Kuwa na wazo bora la biashara unayotaka kuifanya ndiyo msingi mkubwa wa kuweza kufanikiwa katika biashara uifanyayo au ambayo unataka kuifanya. Kuchagua wazo bora la biashara huenda sambamba na kuangalia mahitaji ya watu katika eneo husika.
Kwa mfano kama unataka kuanzisha biashara fulani ni lazima uangalie watu hao wanahitaji nini. Mara baada ya kujua wanahitaji nini ndipo na wewe utapata wazo la kufanya biashara husika. Hivyo wazo bora la biashara hutokea kwa watu wanaokuzunguka.
Zijue siri muhimu za kibiashara ili ukuze biashara yako.
2. Kufanya uchunguzi wa eneo kwa ajili ya kufanya biashara.
Saidi anasema kabla ya kuanzisha biashara yeyete ile ni lazima uweze kutafuta eneo kwa ajili ya kufanyia biashara, na si eneo tu bali ni eneo sahihi kwa ajili ya kufanya biashara husika.
Kuchagua eneo sahihi la kufanyia biashara ni sawa na kuchagua mke bora wa kuoa, kwani endapo utakosea utajilaumu maisha yako yote. Hivyo kila wakati unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unachagua eneo lenye uhakika katika kufanya biashara yenye mashiko kwako.
3. Kutafuta mtaji.
Mara baada ya kupata wazo bora la biashara, na mara baada ya kupata eneo bora kwa jaili ya kufanyia biashara jambo la tatu, unatakiwa kuanza kutafuta mtaji kwa ajili ya kukamilisha wazo ulilonalo.
Majibu ya namna ya kupata mtaji yatapatikana mara baada ya kupata wazo bora la biashara, kwani mahali hapo unatakiwa kufanya uchunguzi yakinifu. Uchunguzi huo utakusaidia kuona kubuni pia namna ya kupata mtaji.
4. Kuwa mbunifu.
Kwa kuwa katika dunia hii kila kitu kinafanana, hivyo ili uweze kujitofautisha na wengine unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unakuwa mbunifu ili uweze kufanikiwa zaidi katika biashara ambayo unaifanya, au biashara ambayo unatarajia kuifanya.
Unapokuwa mbunifu inakusaidia sana kujenga biashara yako na kuifanya biashara hiyo ikaonekana ya mafanikio kwa kupata wateja wengi. Popote pale utakapofanya ubunifu kwenye biashara yako uwe na uhakika utafanikiwa.
5. Kujifunza kwa waliofanikiwa.
Mara baada ya kutafuta mtaji unachotakiwa kufanya ni kujifunza kutoka kwa watu ambao tayari wamekwisha fanikiwa katika biashara husika. Pia Saidi anasema ya kwamba endapo utajifunza kwa watu ambao wameshafanikiwa unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha ni kuwa mbunifu zaidi ya yule ambao umejifunza kutoka kwao.
Lakini anazidi kusisitiza ya kwamba kujifunza ni lazima uweze kusoma vitu mbalimbali ambavyo vitakujenga katika kukuongezea maaarifa katika biashara unayotaka kuifanya. Kwa mfano unaweza ukatembelea mtandao huu wa dira ya mafanikio kila wakati kuna vitu vingi ambavyo vitakujenga sana, endapo utaamua kutenga muda wako kwa ajili ya kujifunza.
6. Unahitaji uvumilivu.
Mara baada ya kuyajua hayo yote, jambo la mwisho ambalo unatakiwa kulifanya ni kuwa mvumilivu. Uvumilivu ndiyo siraha thabiti ya wewe kusonga mbele zaidi. Hivyo ili uweze kufanikiwa zaidi ni lazima uukumbuke ule usemi usemao mvumilivu hula mbivu
0 comentários:
Post a Comment