Fahamu Jinsi ya Kuendesha Biashara Kisomi


  • Kwanza kabla hatujaenda mbali tambua yafuatayo:
  • Sio lazima mwenye biashara awe msomi ili biashara iendeshwe kisomi
  • Sio kila msomi anaweza endesha biashara kisomi.
  • Kuendesha biashara kisomi sio tuu kufanikisha biashara ipate faida.
  • Kuendesha biashara kisomi ni zaidi ya elimu ya darasani ya biashara


Endelea kusoma ufahamu vizuri nini cha kufanya ili biashara iendeshwe kisomi.
Ipo hivi,  kuendesha biashara kisomi ni pale unapoamini na kutenda mambo yahusuyo biashara yako kwa imani na mtazamo kuwa biashara yako ipo sio tuu kwa sababu ya kupata faida ili wewe ujinufaishe bali huko kupata faida ni sehemu tuu ya malipo yako ya kukufanya uihudumie biashara yako ifikie kile ambacho kweli haswa ndio lengo lake.

Hivyo kwa mtazamo wa kisomi ni kuwa pamoja na kwamba wewe unajiita bosi, kiukweli wewe ni mtumishi tuu wa hiyo biashara.

Itazame biashara yako kama kiumbe ambacho kimekwisha zaliwa, kinahitaji kuishi kwa miaka mingi iwezekanavyo. Hata hivyo chukulia binadamu pia kama anaishi tuu ili mradi kukuche, haipendezi. Ndivyo kwa biashara pia. Unahitaji kuikuza, unahitaji kuifanya ionekane na yenywe ya muhimu. Unahitaji kuilinda dhidi ya majanga, na pale inapoumwa (kukosa wateja, au changamoto nyingine za biashara) wewe kama mzazi wake unatakiwa kuisaidia kurudi kwenye afya njema na pia kuikinga isipate matatizo tena.

Hata hivyo wapo pia wazazi wanaozaa watoto wakawatelekeza, wapo wazazi ambao wanazaa watoto ili mradi tuu na wao waseme wana watoto , lakini mpango wa kuwafanya hao watoto wawe kweli wenye kufanya mambo ya msingi kimaisha hawana. Watoto wanaishia kuishi maisha magumu, wengine wanaishia kuuawa kwa wizi.

Hapa tatizo ni mpango-toka mwanzo mzazi hakuainisha nini anataka kufanya kwa ajili ya mtoto wake ( Utasema kila mzazi anamtakia mema mtoto wake, ni kweli, ila neno mema ni neno pana sana. Na pia kutamani sio kutenda). Wakati mtoto anakua, ni jukumu la mzazi kumchunguza mtoto na kumuandalia mazingira ya kuwa mtu bora. Ndivyo kwenye biashara pia, tumesema ichukulie biashara yako kama kiumbe.

Jiulize maswali haya:-
1. Je, ni jambo gani haswa la msingi biashara yako inafanya hapa duniani :
Biashara zote tunazosema zinaendeshwa kisomi ni kuwa zimejifafanua wazi kuwa zipo kutatua tatizo fulani. Zimejifafanua vema ni kwa namna gani zitatatua tatizo hilo. Na vipi zinataka kujulikana katika ulimwengu huu. Maelezo haya ya kusudio la biashara na muelekeo wake  hutajwa katika kitu kinachoitwa MISSION na VISION.

Unakumbuka nilitaja hapo mwanzo kuwa kupata faida sio lazima iwe ndio dalili ya kuendesha biashara kisomi. Ni kweli, wengine wanapata faida kwa dhuluma, kwa hongo, na hata kwa kukandamiza wengine. Kiukweli wengine hawana hata bidhaa kweli halisi wanayozalisha na itakayokuwa endelevu. Ni swala tuu la muda kwamba ni kipindi chao cha “kutesa” au ni kwa sababu ndio wamejikuta wapo kwenye mtandao unaowafanya wawe hapo walipo.
Hii inatuleta kwenye pointi ya pili:

2. Biashara ya kisomi ina mpango kuifanya biashara iwe endelevu.

Mipango na mikakati ya mara kwa mara inafanywa ili kuifanya biashara iweze kujiendesha, iwe kukua na pia isiwe tegemezi kwa maamuzi yasiyo ya kitaalamu. Kufanya biashara endelevu ni pamoja na kuhakikisha kuwa biashara ina akiba ya kutosha, ina uongozi wenye kuelewa biashara inaendeshwaje, na kuthamini utaalamu.

Nakumbuka tuliwahi kuanzisha biashara na jamaa kadhaa ilikuwa ni wasomi tupu toka UDSM na kweli kwa simu za mwanzo tulipata fedha hata hivyo hatukuwa na mipango endelevu na uongozi wenye kuheshimu biashara. Ilikuwa ili mradi tuu tupate hela tugawane siku ziende. Najua bado zipo biashara nyingi za namna hii zipo ndogo vile vile au zinakaribia kufa. Au la zinaleta presha tuu kwa wamiliki.

3. Biashara inayoendeshwa kisomi imemuweka mteja kwanza:

Mteja ndio haswa bosi wa kweli kwani yeyé anaweza kumwachisha kazi hata mmiliki wa biashara (Subiri biashara yako ikose wateja uone kama hautofunga). Hivyo biashara ya kisomi ili ibaki kuwa endelevu inabidi itumie muda wa kutosha kujifunza tabia, mahitaji na uwezo wa wateja katika kununua bidhaa. Inahitaji pia kujenga mahusiano bora, na zaidi sana kuwa na mbinu za kufikia wateja wapya zaidi na zaidi.

Biashara inayoendeshwa kisomi inazingatia kuwa na bidhaa sahihi:  Ndio ukweli ulivyo, kwamba ili wateja waendelee kukuajiri inabidi uwe na kitu sahihi cha kutatua mahitaji yako. Hivyo basi ni muhimu kuwa na bidhaa yenye kutimiza mahitaji ya wateja wako. Na kama alivyowahi kusemaKumbuka maneno haya ya Seth Godin, gwiji wa marketing :

"Quality doesn't mean perfection. It means keeping the promise the customer wants you to keep. "
Yaani:  Ubora wa bidhaa hauna maana utengeneze kitu kisicho na mapungufu , bali ina maanisha kuwa utimize ahadi ambayo mteja anataka uitimize.

4. Biashara inayoendeshwa kisomi inazingatia kuwa na usimamizi ulio imara:
Usimamizi imara hapa unaanza kwanza kwenye ujuzi wa bidhaa husika inayozalishwa au kuuzwa, pia ujuzi wa mambo mengine ya msingi kama vile usimamizi wa fedha, usimamizi wa wafanyakazi, mawasiliano sanifu,  ujuzi wa masoko,  uwezo wa kuweka mipango, kodi, na ujuzi wa kusoma mazingira na mabadiliko katika jamii ili kuweza kuendana na mabadiliko. Sio lazima mmiliki wa biashara ajue yote haya, ila anaweza kuajiri watu wenye ujuzi wa mambo husika wamsaidie
Share on Google Plus

About Admin

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comentários:

Post a Comment