Kuonekana umefanya makosa mbele za watu ni kitu kinachotishia utambulisho wa mtu, ndiyo maana watu wengi wanachukulia kufanya makosa kama jambo la kurudi nyuma. Mtazamo wa waliowengi ni kwamba kwenda mbele ni pale tu wenzako wanapokuona uko sahihi kwa mtazamo wao binafsi. Kutaka kuonekana sahihi mbele ya macho ya wenzako ndiyo usababisha hali ya kupenda kila mara kujihami, kujilinda, kulaumu watu wengine au kusingizia kitu kingine, hasa pale inapotokea mambo yemekwenda ndivyo sivyo.
Matokeo yake na bila kujua unajikuta unakuwa mtumwa wa watu wengine wanageuka kuwa mabosi wako. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kila jambo inabidi uwasikilize wao wanasemaje unapata ruhusa kutoka kwao.
Endapo ukifanya jambo la lenye manufaa kwako na kwa watu wengine lakini wale watu wako wa karibu wakasema siyo sahihi, basi wewe utaliacha “eti kwasababu watu wanasema siyo zuri”.
Unapokuwa mtu wa kuongozwa na maoni kutoka kwa watu wengine, ujue kuwa muda si mrefu utaanza kupoteza ubunifu wako. Kwa sababu, kila wakati unafanya kazi zako kwa tahadhari sana, ukilenga kutoonekana mbaya. Hofu ya kufanya kazi kwa kuogopa kuonekana mbaya ikizidi, kinachofuata ni kuziba kwa mfereji wa ubunifu kutoka kwenye akili yako.
Kuziba kwa mfereji maana yake ni kwamba, juhudi na akili zako hazijikiti tena kwenye kutafuta suluhisho kwa changamoto na matatizo yaliyopo, bali kwa kiwango kikubwa utatumia akili nyingi katika kufanya vitu ambavyo unadhani watu wako wa karibu watakupongeza au kukusifu.
Mtu anayependa kuonekana sahihi pia ni mtu asiyeamini kama kuna mtu mwingine anaweza kufanya vizuri zaidi ya yeye. Huyu ni mtu asiyeamini vipaji vya watu wengine. Siku zote anaamini asipofanya yeye hakutakuwepo na matokeo mazuri. Kila mara anakuwa ni mtu wa kujisemea rohoni ya kwamba“bila mimi kuwepo mambo hayawezi kwenda".
Ukweli ni kwamba bidhaa au huduma yoyote ile tunayoiona sokoni haiwezi kamwe kutolewa na mtu mmoja, kwa sababu hakuna binadamu anayeweza kuwa na vipaji vyote.
Tabia ya kupenda kuonekana sahihi kwa watu, kwenye biashara na uwekezaji haifai. Hii ni kwa sababu, kwenye biashara na uwekezaji tunaamini sana katika kuunganisha vipaji vya watu mbalimbali (timu) kwa lengo la kuzalisha suluhisho kwa changamoto na matatizo yaliyopo kwenye jamii. Tunafanya hivyo kwasababu, bidhaa na huduma unazotumia leo hii, ni matokeo ya vipaji mbalimbali vilivyounganishwa pamoja na mfanyabiashara au mwekezaji.
Katika nyanja nyingine za maisha, kuongezeka kwa watu ambao wanakupongeza na kukusifu hakuleti faida ya moja kwa moja kwako, kama ipo. Na mara nyingi ukifanikiwa kupata faida, inakuwa siyo ya kudumu. Wakati huohuo, hali ya nyanja za maisha ya biashara na uwekezaji ni tofauti kidogo na uko kwingine. Kwenye biashara, mpango mzima ni kuelekeza juhudi na akili kwenye kuzalisha, kuongeza, na kutoa thamani kubwa kwa watu wengine.
Kwenye biashara hasa kubwa, wateja ndio rafiki zetu wa karibu na ndio kipimo cha usahihi wa kile tukifanyacho. Jukumu kubwa ni pamoja na kuendelea kujituma na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa mpaka pale wateja wanaporidhika. Uzuri wa kufanya kazi kwa lengo la kuridhisha wateja wako ni kwamba, wale wateja wanaoridhika na kazi unayoifanya wanavyozidi kuongezeka, ndivyo kipato chako kinavyozidi kuongezeka pia.
Kama unataka kuwa mfanyabiashara na mjasiriamali mkubwa, anza leo kujiwekea mazingira ya kufuta tabia hii ya kupenda kila wakati kuwafurahisha watu. Kamwe usitake kuwa sahihi kwa ajili ya watu wengine, bali kuwa sahihi kwa ajili ya wewe mwenyewe binafsi, pia kufanya yale unayotakiwa kufanya. Usipoacha tabia hii ya kila wakati kutaka kufanya vitu vinavyokuthibitisha kwao kuwa wewe una uwezo mkubwa, nakuhakikishia kuwa haitatokea hata siku moja ukafanikiwa kwenye biashara
0 comentários:
Post a Comment